Polisi wapambana na waandamanaji wa upinzani Venezuela


Kiongozi wa upinzani Venezuela Juan Guaido alitangaza jana maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali wakati maelfu ya watu wakimiminika katika barabara za mji mkuu Caracas kumuongezea mbinyo Rais Nicolas Maduro.

Guaido aliwaambia maelfu ya wafuasi wake kuwa atafanya ziara ya nchi nzima kabla ya kuongoza maandamano makubwa katika mji mkuu.

Guaido, spika wa bunge mwenye umri wa miaka 35, ambaye anatambuliwa na zaidi ya nchi 50 kuwa rais wa mpito, alitishia kuomba msaada kutoka nje wakati muda utakapowadia akiinukuu katiba ambayo inaruhusu matumizi ya jeshi la Venezuela linalohudumu nje ya nchi, au raia wa kigeni walioko nchini humo.

Maduro pia aliwataka wafuasi wake kuupinga "ubeberu" katika maandamano ambayo yanaashiria miaka minne tangu Marekani ilipoitangaza Venezuela kuwa "kitisho" kwa usalama wake na kuiwekea vikwazo.

 Hayo yalijiri wakati mamlaka zikijaribu kurejesha huduma za umeme ambazo zilikatika tangu Alhamisi mchana