3/17/2019

Pombe yatajwa sababu askari aliyefia baa


Uchunguzi wa kitabibu wa mwili wa askari, PC Donald Motoulaya (29) wa ofisi ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma uliofanywa na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Songea (Homso), umebaini kuwa kifo chake kilitokana na kunywa pombe kupita kiasi.

Askari huyo alikutwa amefariki dunia Machi 13, saa 4:30 asubuhi katika baa ya Friends Pub iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Machi 14, siku moja baada ya kutokea kifo hicho, kamanda wa Polisi mkoani hapo, Simon Marwa alisema kabla ya kifo Motoulaya alianguka kwenye ngazi za mlango wa baa baada ya kujikwaa.

Jana, Mwananchi lilizungumza na kaimu mganga mfawidhi wa Homso, Dk Hassan Rumbe aliyesema mwili wa askari huyo ulipelekwa hospitalini hapo na watu wasiofahamika na kupokewa na mganga wa zamu.

Alisema mwili huo ulifanyiwa uchunguzi na kubainika Motoulaya alifariki dunia muda mrefu na madaktari walikuta akiwa na mchubuko mdogo katika shavu la kushoto, huku sababu ya kifo chake ikithibitika kuwa ni kunywa pombe kupita kiasi.

Kwa upande wake, Kamanda Marwa alisema mwili wa askari huyo ulisafirishwa juzi kwenda Makambako mkoani Njombe kwa ajili ya mazishi.

Alisema, awali mmoja wa wahudumu wa baa alimtoa nje askari huyo baada ya kubaini kuwa amelewa akitokea katika baa nyingine iliyopo jirani huku akitaka kinywaji zaidi.

“Baada ya kutolewa nje huku mhudumu akiendelea na shughuli zake, askari huyo alijipenyeza na kuingia kwenye chumba cha ndani cha baa hiyo na kwenda kukaa eneo lililowekwa makochi. Huyu askari alikuwa ameyazoea mazingira ya baa hiyo, hivyo alikaa huko bila wahudumu kufahamu kama yupo,” alisema Marwa.

Alisema wahudumu wa baa hiyo walipokuwa wakifanya usafi asubuhi walibaini kuwa kuna mtu kwenye kochi amelala na baadaye iligundulika kuwa amefariki dunia.