Serikali ya New Zealand kuanza kutoa miili ya waliokufa


Mamlaka za New Zealand zinatarajia kuanza kukabidhi miili ya watu waliokufa kwenye shambulizi la misikiti miwili nchini humo, wakati hii leo zitakapoanza kutoa mwili wa kwanza kati ya miili hiyo 50.

Wachunguzi wa vifo wamesema wanatarajia kutoa angalau mwili mmoja leo Jumapili na kuziruhusu familia zinazosubiri kwa hamu kuwazika jamaa zao kwa kuzingatia imani yao ya kidini.

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Arden amesema miili ya waliokufa itaanza kutolewa baadae jioni na kuongeza kuwa wanataraji hadi siku ya Jumatano watakuwa wameikabidhi miili yote kwa familia zao.

Akizungumzia shambulizi hilo Arden amesema yeye pamoja na maafisa wenzake 30 walipewa taarifa kupitia barua pepe dakika tisa kabla ya kufanyika shambulizi hilo. Hata hivyo Arden aliongeza taarifa hiyo haikutaja eneo na haikuwa na ufafanuzi zaidi, na ilitumwa pia kwa idara ya ujasusi.