3/17/2019

Soko la dhahabu Geita lazinduliwa na Waziri Mkuu


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezinduliwa soko kuu la dhahabu mkoa wa Geita leo baada ya kumaliza ukaguzi wa mabanda yatakayotoa huduma ndani ya soko hilo. Waziri Mkuu alikuwa ameongozana na Waziri wa Madini, Dotto Biteko pamoja na watendaji mbalimbali wa taasisi mbalimbali za serikali.

Katika uzinduzi huo Waziri Mkuu ametembelea na kuhoji masuala mbalimbali katika banda la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), litakalotoa huduma mbalimbali ikiwamo uthibitishaji wa thamani halisi ya mapato yatokanayo na madini kwa wauzaji wa madini.

Ametembelea banda la kamati ya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuimarisha usalama kwa wafanyabiashara na wadau wa soko hilo. Pia alitembelea katika mabanda ya benki za NMB na CRDB zilizojipambanua namna zitakavyohusika katika ufanikishaji wa huduma za kifedha ndani ya soko hilo.

Soko hilo litakalofungua fursa za kiuchumi kwa mkoa huo, litahusisha wadau wote walio kwenye mnyororo wa biashara ya madini wakiwemo wanunuzi, wauzaji, TRA, Tume ya Madini, benki na mamlaka ya serikali za mitaa.