UNICEF yaonya muda unakwisha kwa wahanga wa kimbunga Msumbiji


Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF Henrietta Fore ameonya jana kwamba juhudi za kiutu zinazidi kuchelewa kwa mamia kwa maelfu ya watu wa Msumbiji waliathirika na kimbunga Idai kilichopiga wiki iliyopita.

 Fore amesema muda unakwisha , na imefikia katika wakati mgumu. Amesema hayo muda mfupi baada ya kuwasili katika mji wa bandari ulioharibiwa na kimbunga hicho wa Beira kutoka New York kutathmini hali katika mji huo.

Umoja wa mataifa umeanzisha miito ya kuomba msaada wakati ukisubiri taarifa za kutosha kuweza kutoa makadirio sahihi ya mahitaji wakati operesheni za uokozi zikiendelea.

Amesema kwamba hatua inayofuata ni kupata maji safi ya kunywa kwa sababu magonjwa ndio kitu kitakachofuatia kwa sababu kuna maji yaliyotuwama, miili iliyoharibika na kuoza, ukosefu wa vyoo na vifaa vya usafi wa mwilini.