Vazi la kitenge linavyokuweka 'smart'

Ni miaka mingi sana sasa, Afrika imekuwa ikitengeneza malighafi hii ya Kitenge. Mataifa mengi kama Nigeria, Ghana, DR Congo na kwingineko, tulizoea kuwaona wakivaa vitenge vilivyoshonwa kwa mitindo anuai na ya kuvuatia.

Hapa nchini Tanzania, Kitenge, naweza kusema kimechelewa sana kupewa nafasi ingawa tulikuwa na viwanda vilivyozalisha aina hii ya malighafi kama Sunguratex, Urafiki nk. Nyakati zile ilikuwa ukimwona mwanamama kavaa vazi hilo basi moja kwa moja watu watasema ‘kavaa vazi la taifa’.

Halikuwa vazi la kawaida, kwa sababu tulitekwa na mitindo mingi ya kigeni. Wanaume ni wachache sana ambao walivaa vazi hili miaka hiyo.

Lakini sasa mambo yamegeuka, Kitenge kimekuwa vazi la gharama na kinashonwa katika mitindo mbalimbali ya kuvutia kama magauni, mashati, kaptula, suruali, suti, mikoba na ushishangae ukikutana na viatu vya aina hii.

Hakika ukivaa muonekano wako hubadilika, urembo au ushababi wako huwa dhahiri shahiri hasa ukimpata fundi anayejua vyema kucheza na ‘body’ na kukufyatulia kitu kifaacho. Vijana watasema ‘Amazing!’