3/15/2019

Wananchi wa Babati wasisitizwa kulima zao hili ili kujikomboa katika umaskini


Na. John Walter,Babati

Mbunge wa Babati Vijijini mkoa wa Manyara Jitu Soni (CCM) amewataka wananchi wa Kijiji cha Guse, Kata ya Bashnet Wilayani Babati Mkoani Manyara kulima zao la biashara la pareto ili kujikomboa katika umasikini .

Alisema kwa kuwa kijiji hicho kipo ukanda wa baridi na ukanda huo hauwezi kuzalisha mazao mengine ya biashara ya mbaazi  na alizeti yanayozalishwa kwa wingi Wilayani humo  hivyo wanapaswa kupanua mashamba yao kutoka mashamba madogo kuja mashamba makubwa kwa kulima zao la biashara la Pareto.

Akizungumza na wananchi hao kupitia mkutano aliouitisha Mbunge huyo wa jimbo la Babati Vijijini   Jitu Son, Kwa mujibu wake Pareto kama zao la biashara linalostawi katika eneo la ukanda wa baridi litawasaidia wananchi hao kuondokana na mazoea ya kulima mahindi na viazi pakee kwa ajili ya mazao ya kujikimu.

Alibainisha kuwa kilimo cha pareto kitachangia pia uchumi wa viwanda kwani kutakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana, akina mama watakajipatia kipato cha kujikimu katika maisha yao na kuwapa elimu watoto wao.

“Hili ni zao zuri kwa ajili ya biashara ikishaanza kutoa maua inavunwa kila baada ya wiki mbili, vijana  na kinamama mnaweza kujiunga  katika vikundi mkatafuta mikopo na kukodisha shamba ili mlime Pareto kwa  kujipatia kipato kwa urahisi zaidi na itawasaidia katika kusomesha, na matumizi ya haraka mkaacha kutegemea mahindi  na viazi  ” alisema Jitu.

 Mkurugenzi wa Kampuni ya Pareto Tanzania ya Pyrethum Company of Tanzania Ltd (PCT) yenye makao yake Iringa na inayojishughulisha na kununua Pareto nchini  imewahakikishia wananchi  wa Kijiji cha Guse, kuwa itanunua  pareto yote itakayolimwa katika msimu wa mwaka 2019/2020.

Mkurugenzi huyo  John  Power alisema kampuni hiyo ipo tayari kununua  pareto  yote itakayozalishwa kwa ubora  kwa shilingi 2300 hadi 3000 kwa kilo moja.

John Power  aliwataka wananchi hao kuendelea kulima kwa wingi zao hilo na kwamba Kampuni hiyo ina uhitaji  mkubwa wa Pareto na inaweza kununua kiasi chochote kitakacholimwa.

“Endeleeni kulima hata kama ni shamba dogo kadri mnavyozidi kupata faida ndio mtaongeza mashamba , sisi tunawahakikishia uhakika wa soko, hatujawahi kufeli kununua hata kilo moja ya pareto kutoka kwa mkulima” alisema Power.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Guse John Gwandu alisema wananchi wameanza kulima kwa wingi baada ya kuona  manufaa kwa wachache walioanza kulima zao hilo kwani maisha yao yalibadilika na waliweza kulipa hata michango ya kijiji kwa haraka kwakuwa waliuza pareto., tofauti na zamani ambapo walitegemea viazi tu.

“Wananchi wamepata hamasa ya kulima zao hili kwasababu wale walioanza walipata mafanikio, wengine wanaendelea kuongeza mashamba kila siku, sasa hivi miche mingi ipo kwenye bustani  wananchi wengi wanaendelea kuongeza mashamba ili kuongeza pato lao” alisema Gwandu.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Getabuske  kijiji cha Guse  Baltazari  Petro  alibainisha kuwa kwa mara ya kwanza  zao hilo limeanza kulimwa  mwaka huu  na wananchi  wengi  wameitikia wito  wa kupanua mashamba yao ingawa changamoto  iko  katika upatikanaji  wa miche.

Kupitia wakala wa ukusanyaji  wa pareto kijijini hapo  alibainisha kuwa wakulima wengi wamekuwa wakipeleka  mazao yao katika kituo  cha wakala  huyo  na kulipwa  fedha  zao  kulingana na ujazo  unaotakiwa pasipokuwa na usumbufu wowote.

“Kwa mwaka tunalima misimu miwili  ya miezi mitatu, mwaka jana ni wakulima kumi tu walilima Pareto kwa kiwango  kidogo  baada ya kuona uhakika wa soko  wengi wamepanua mashamba yao” alisema Petro.

Katika mkutano huo   Mbunge huyo  alitoa mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho na  Mkurugenzi wa kampuni ya Pareto Tanzania alitoa mifuko 10 ya saruji kama sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya kijiji hicho.