Watumishi wa sekta ya Ujenzi watakiwa kuongeza ubunifu


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kuongeza ubunifu na bidii katika kazi wanazozifanya ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani.

Mhandisi Kamwelwe, amesema kuanzia sasa wafanyakazi wa sekta hiyo wawekewe mkakati utakaowapa fursa za kutosha kujiendeleza kitaaluma ili kuwezesha Wizara na Taifa kuwa na wataalam wakutosha wenye ubunifu wa kisasa na hivyo kuhakikisha miradi inayosimamiwa na Serikali inakuwa yenye ubora.

Akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara yake mjini Dodoma Mhandisi Kamwelwe amehimiza umuhimu wa kila mfanyakazi katika Wizara hiyo kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika eneo lake la kazi ili kuhakikisha kazi zinazofanywa zinapimika na kuleta tija.

“Hakikisheni watumishi wanaendelezwa kila wakati ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayotokea sasa duniani kote,” amesisitiza Waziri Kamwelwe.

Amezungumzia umuhimu wa wafanyakazi kusikilizwa na kupewa motisha pale wanapobuni masuala yatakayoisaidia sekta ya ujenzi katika kukuza teknolojia na kuzingatia thamani ya fedha ili kuwezesha nia ya Serikali ya kuwa na wataalam wengi katika miradi mikubwa ya ujenzi nchini kufikiwa.


Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items