Waziri Lugola ataka biashara haramu ya binadamu izidi kudhibitiwa


Na Felix Mwagara, MOHA-Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameitaka Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu nchini, iongeze kasi ya kupambana na biashara hiyo ili iweze kudhibitiwa kwa kuwa inaichafua nchi.

Waziri Lugola ambaye kesho anatarajia kufungua mkutano mkubwa wa mafunzo kwa watekelezaji wa sheria ya kuzuia biashara hiyo haramu, katika hoteli ya Ngalawa, mjini Unguja, Zanzibar, alisema hayo wakati akijiandaa kufungua mafunzo hayo, lakini wahusika waweke mikakati thabiti ya kuidhibiti biashara hiyo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Waziri Lugola alisema Mkutano huo ni muhimu kwa wadau hao kupata mafunzo ya kukabiliana na mapambano ya biashara hiyo haramu ambayo Wizara yake itaendelea kuidhibiti.

“Nimealikwa kufungua mkutano huo, baada ya mafunzo hayo ya kitaalamu ambayo nimeambiwa yatakuwa ya siku tano, naamini maafisa watakaopewa mafunzo hayo kutoka Wizara yangu na maafisa wengine wa Serikali kutoka sehemu mbalimbali nchini, pamoja na NGO’s za hapa Zanzibar watakuwa wamepikwa na kuiva na hatimaye watatusaidia katika kutekeleza sheria ya kuzuia biashara hii haramu ya usafirishaji wa binadamu,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara hiyo Haramu kutoka Wizara hiyo, Separatus Fella, alisema zaidi ya washiriki 80 watapewa mafunzo hayo na anamatarajio makubwa elimu watakayopewa itazaa matunda.

Fella alisema washiriki watapewa mafunzo mbalimbali katika semina hiyo itakayofanyika Kesho Machi 25, 2019, ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa zikiwemo, washiriki kujua kutofautisha makosa ya biashara haramu ya usafirishaji binadamu na mengine, na namna ya kupeleleza na kuendesha mashtaka.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items