Na John Walter, Manyara
Kuharibu mazingira na vyanzo vya maji ndio sababu kubwa ya kukosekana kwa mvua katika maeneo mengi na kupelekea kutokea kwa ukame hapa nchini.
Hayo yamesemwa leona Sheikh mkuu wa mkoa wa Manyara, Mohammed Khamis Kadidi Katika Dua maalum ya kuomba Mvua katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati ambapo amewataka waumini wa dini ya kiislam kuzidisha maombi na kutenda yaliyo mema ili Mwenyezi Mungu asikie dua zao na kuleta mvua yenye baraka.
Amesema panapotokea hali ambayo inatishia uhai wa mwanadamu kama ukame, dini ya Kiislamu inaelekeza kumrejea Mungu kwa kufunga Swaum za Sunna na kuswali ili Mwenyezi Mungu pekee aweze kubadilisha hali hiyo.
"Ili Mungu atuhurumie ni lazima tuwalee watoto katika maadili ya kidini kwa kuwapeleka madrasa ili watambue namna Quran inavyoelekeza kutenda mema," alisema Shekh Kadidi.
Waislamu kote nchini leo wamefanya ibada maalumu ya kuomba mvua kutokana na ukame unaoendelea maeneo mbalimbali nchini na kupelekea mazao kukauka hali inayoeleta hofu kwa wawananchi haswa wakulima. Dua hiyo kitaifa imefanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir.
