Zanzibar kutoa ushirikiano kwa Shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki duniani


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohamed Said amesema Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kwa shirika la nguvu za atomiki Duniani ili kukuza na kuimarisha teknolojia ya utumiaji wa mionzi.

Ameyasema hayo katika mkutano wa pamoja na ujumbe wa shirika la Nguvu za Atomic Duniani (IAEA) kanda ya Afrika, Simai amesema Zanzibar Bado ipo chini kwa utumiaji wa Teknolojia ya mionzi.

Aidha ameutaka ujumbe huo kuunganisha nguvu na Wizara ya Elimu kupitia chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili nao waweze kutoa Elimu kuhusiana na matumizi ya Teknolojia ya mionzi.

Nae Mkurugenzi wa shirika la nguvu za atomic Duniani (IAEA) kanda ya Afrika Profesa Shaukati Abdulrazak amesema malengo hasa ya IAEA ni kutumia Teknolojia katika uzalishaji wa vyakula, kuondoa wadudu waharibifu wa mazao na kupambana na maradhi ya saratani.

Aidha amesema shirika la IAEA lipo tayari kuwajengea uwezo wazanzibar ili waweze kutumia Teknolojia kwa lengo la kuleta maendeleo zaidi.

Pia amesema Teknolojia hiyo ni kuhakikisha kila chakula ni salama kwa matumizi ya kibinaadamu.

Alisema wataendeleza ushirikiano ili kuhakikisha Zanzibar nayo inapata kifaa cha kupimia maradhi ya saratani.

Nae Mkurugenzi mkuu wa tume ya Nguvu za Atomic Tanzania (TAEC) Profesa Lazaro Busagala amesema kwa kazi ya majaribio ya mwanzo ya shirika hilo la Zanzibar ni kuhakikisha hakuna kabisa wadudu wa Mbung'o, zoezi ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Aidha amesema ushirikiano mzuri ndio utakaosababisha wazanzibar kuendelea mbele kiteknolojia.