Rais wa Algeria kunga'atuka mamlakani


Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika ataachia wadhifa wake huo Aprili 28, kabla ya kumalizika kwa muhula wake wa nne. Ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya washirika wake wa karibu kujitenga naye

Ni hatua ambayo imechukuliwa katika wakati ambapo pia kuna maandamano makubwa ya raia ya kumshinikiza kiongozi huyo mdhaifu kung'atuka.

Bouteflika mwenye umri wa miaka 82, ambaye pia amekuwa akionekana mara chache hadharani tangu alipopatwa na kiharusi mnamo mwaka 2013, amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu mamlakani, kutokana na kuongezeka kwa shinikizo kwa wiki kadhaa baada ya jaribio lake la kutaka kusalia madarakani baada ya miaka 20 ya utawala.

Bila ya kutoa maelezo zaidi, taarifa kutoka ofisi ya rais imesema Bouteflika atajiuzulu kabla ya Aprili 28, baada ya kuchukuliwa kwa kile kilichotajwa kama "maamuzi muhimu".

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na shirika rasmi la habari nchini humo la APS imesema Bouteflika atachukua kwanza hatua zinazolenga kuhakikisha taasisi za serikali zinaendelea kufanya kazi zake katika kipindi cha mpito.

Rais wa chama cha upinzani cha UCP Zoubida Assoul amezungumzia hatua hiyo ya rais Bouteflika, kwenye mahojiano na shirika la habari la AFP. Alisema "Sitaki kumsubiri hadi atangaze kujiuzulu kwa sababu tunajua kwamba anatakiwa kuondoka mamlakani ifikapo Aprili 28. Kwa hiyo sio tukio la kushangaza na wala halikutangazwa kwetu kama kitu kikubwa. Tungependa atuambie anarejea kwenye mkakati wake uliokataliwa na watu na hata upinzani, ikiwa ni pamoja na mimi."
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items