Harakati za Khalifa Haftar ni za kimapinduzi



Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema mienendo na harakati zinazofanywa na Jenerali Khalifa Haftar na vikosi vyake ni za kimapinduzi na wala hazifanani na harakati za kupambana na ugaidi kama anavyodai yeye.

Ghassan Salame ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la BBC na kuongeza kuwa, "Kitendo cha Haftar cha kutoa waranti wa kukamatwa Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa na maafisa wengine wa serikali hiyo inaelekea kuwa ni hatua za kufanya mapinduzi na wala sio kupambana na ugaidi."

Mjumbe huyo wa UN nchini Libya amebainisha kuwa, "Hakuna upande unaoweza kufanikiwa kupata nguvu za kijeshi dhidi ya upande wa pili. Hii leo tupo katika mgogoro wa kijeshi kwa siku ya nane au tisa."

Huku hayo yakijiri, Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika mashambulizi ya vikosi vya Haftar vya kutaka kuudhibiti mji mkuu wa Tripoli imeongezeka na kufikia watu 147 huku wengine 614 kujeruhiwa.

Hali kadhalika Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limeonya kuwa, kushtadi kwa mapigano hayo ya Libya kutapelekea kuongezeka idadi ya wakimbizi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Jenerali muasi Khalifa Haftar ametupilia mbali wito wa kimataifa unaomtaka asitishe mapigano dhidi ya wapiganaji tiifu kwa serikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli na inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.