F Hatua muhimu za kuzingatia wakati wa kuandaa mchanganuo wa biashara | Muungwana BLOG

Hatua muhimu za kuzingatia wakati wa kuandaa mchanganuo wa biashara

Watu wengi hupenda kuandaa au kuanzisha biashara bila kufuata taratibu stahiki. Biashara yenye mafanikio ni ile iliyoanzishwa kwa taratibu za kitaalamu na kuandikiwa mchanganuo, japo wengi ufikiri mchanganua ni kwa ajiri ya kuchukulia mikopo, la hasha sio kweli mshanganuo ni dira na mwongozo.

Kuna hatua tano za kupitia unapotaka kuandika au kuundaa mchanganuo wa biashara kama ifuatavyo;

Kuwa na wazo.
Jambo la kwanza kabla ya yote unapotaka kuanza kufanya biashara au kuandika mchanganua wa biashara ni kuwa na wazo. Vijana wengi tuna ndoto za kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Huwa tuna mawazo mengi kwa wakati mmoja ambayo hatuwezi kuyafanyia kazi, hivyo upelekea kukosa mwelekeo.

Wengi utawasikia wakisema mtaji ndio kikwazo lakini kikwazo kikubwa sio mtaji pekee, kikwazo kinaweza kuwa ni WAZO, wazo sahihi ndio msingi mkuu katika kufanya ujasiliamali. Wazo linaweza kuwa la kuiga, kuboresha au jipya kabisa ambalo unafikilia kulifanyia kazi. “Miluzi mingi upoteza Mbwa” usemi unamaana sawa kabisa na kusema mawazo mengi hupoteza malengo,vijana wengi tuna mawazo mengi ambayo hatuwezi kuyafanyia kazi.

Kitu cha kwanza ni kuchuja mawazo mengi na kuchagua wazo moja au kuangalia lipi la kuanza nalo ,na kuangalia kama linaweza kutekelezeka. “Screening Business Ideas” . Kuangalia kama bidhaa au huduma inahitajika sehemu husika ?.Kuangalia kiwango cha ushindani wa biashara au huduma katika eneo husika.

Wengi huwa na mawazo mazuri lakini huyapanda katika mazingira yasiyo sahihi ambayo upelekea kushindwa kuzifanya biashara hizo, na hatimaye mawazo hayo kunyauka na kufa.

Mjasiriamali anapotaka kufanya biashara uchagua wazo moja lenye nguvu, ambalo linaweza kustawi katika mazingira husika, na kulipanda. Mtu mwenye mawazo mengi kwa wakati mmoja na yote anayafikiria kuyafanyia kazi kwa wakati mmoja, huyo sio mjasiliamali kwa kuwa ameshindwa kujiamini kwa kusimama na wazo moja.

Utafiti wa soko.
Kufanya utafiti wa soko la biashara ulioichagua kuifanya. Utafiti ni jambo la msingi sana kwa mjasiriamali kabla hajafungua biashara yake. Utafiti unahusisha kukusanya taarifa muhimu juu ya soko, mauzo ,usambazaji ,utangazaji wa bidhaa zitakazozalishwa.

Kujua ni aina gani ya wateja wako, kuzingatia Umri, jinsia, kipato chao, elimu yao, na dini zao. Mfano ni ajabu kwa mjasiliamali kuuza midoli kwenye jamii ambayo 95% ni watu wazima(Wazee). Ni ajabu kwa mjasiliamali kuuza majaketi ya baridi Dar es salaam, badala ya kupeleka Makambako, Iringa au Kilimanjaro.
Kuna nguo ukienda kuuza Zanzibar soko lake ni finyu sana lakini nguo hizo hizo ukiuza Dar es- salaam zitanunulika sana. Hapo namaanisha kuwa zipo bidhaa ambazo zitakosa soko kwa kuwa umewapelekea jamii fulani bila kuzingatia mambo hayo ya msingi . Hapo utakuwa umeanzisha biashara kwa kutofwata misingi ya kijasiliamali.

Eneo la kuwekeza
Wapi biashara iwekwe. Hili ni tatizo kubwa sana linalowakuta wajasiriamali. Kupata eneo ambalo unaweza kupata vyanzo vya uzalishaji “Factor of productions ”.Je kuna rasilimali, wafanyakazi, wateja, kiwango cha kodi, taasisi za kifedha nk. Je ni kuna miundo mbinu rafiki? . Je Teknolojia ni rafiki kwa aina ya biashara inayotaka kupandwa?.

Uongozi na utawala.
Ili biashara iweze kusimama vyema inahitaji usimamizi mzuri. Usimamizi bora ndio chachu ya kufanikiwa katika biashara yoyote ile. Vitu vya kuzingatia ni kuwa na watu ambao wana ujuzi na moyo wa kufanya biashara hiyo. Wenye kuzingatia misingi ya kijasiliamali. Je una watu wa aina hiyo?

Mchanganuo wa fedha.
Baada ya mipango yote hapo ndipo tunaangalia pesa itapatikana wapi na itasimamiwa vipi. Ni mara chache sana kusikia mtu akizungumzia jinsi vyanzo vingine vinavyotakiwa kuzingatiwa kuliko mtaji.

Ni kweli kuwa mtaji ni kitu muhimu lakini bila kuzingatia haya mengine mtaji utakua na faida gani. Watu wengi wanakimbilia kuchukua mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara zao ila ni wachache wanaofanikiwa kusimamisha biashara hizo.

Hatima yao ni kupokonywa vitu vya dhamani ambavyo waliweka rehani. Ili uweze kufikiria mtaji inabidi uyafanyie kazi hayo mengine ya awali, hapo ndipo utajua ni kiasi gani cha mtaji kinachohitajika na ukisimamie vipi.

Katika mchanganuo wa fedha unatakiwa uainishe chanzo cha mtaji, jinsi utavyoutumia huo mtaji kukamilisha malengo yako. Lazima kuweka taarifa za muhimu ambazo zitakuwa mwongozo katika kusimamia mtaji. Hilo ni jambo la msingi la kuzingatia kwa wajasiliamali.
Faida ya biashara.
Hakuna biashara inayofanywa bila kuzingatia faida. Faida ndio kiini na sababu ya kufanya biashara. Wajasiliamali wengi wanapoanza biashara hutegemea faida, lakini sio biashara zote zinatoa faida kwa wakati. Pia zipo biashara ambazo hazitoi faida hivyo zinapelekea kufungwa.

Kipimo cha matazamio ya biashara ni miezi takribani sita hivi kama wanavyoshauri wataalamu. Baada ya hapo kama hakuna faida inabidi urudi nyuma na kuangalia ni hatua ipi haijazingatiwa. Hapo ndipo mjasiliamali anatakiwa kujipanga pale atapofikiria kuanza kufanya biashara yake mwenyewe kwa kufuata misingi ya kijasiliamali.