IGP Sirro awataka Polisi kuacha kuwanyanyasa raia


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amewataka askari wa jeshi hilo kuacha kupokea rushwa na kutonyanyasa raia.

IGP alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na viongozi wa jeshi hilo Mkoa wa Morogoro.

Alisema hayo kwenye ziara ya ghafla ya ukaguzi wa ujenzi wa nyumba za askari zilizojengwa kutokana na michango, iliyowashirikisha wadau wa maendeleo.

 Alisema watu wakifanya kazi bila woga, kutokana na kuwepo kwa usalama wao na mali zao, wanakuwa mstari wa mbele kuliunga mkono jeshi lao, kama wadau wengi hivi sasa wanavyotoa michango yao ili kujenga na kukarabati nyumba za askari wa Morogoro.

Kwa upande wa ulinzi na usalama wa raia kwa Morogoro, alisema Mkoa wa Morogoro ni shwari, ila wananchi wasibweteke, kwa sababu hata matukio yaliyotokea Kibiti mkoani Pwani, historia yake inaonesha yalianzia kwenye mapori ya Morogoro. "Watu wachache wanaotaka kutuletea shida bado wapo, ni vyema kila mmoja wetu kumjua jirani yake na pale unapomtilia shaka ni vyema kutoa ripoti kwa vyombo vya ulinzi na usalama hasa Polisi," alisema IGP Sirro.