Madaktari wawili kutoka Cuba waliotekwa na Al Shabab Kenya waendelea kusakwa


Hatima ya madakatari wawili raia wa Cuba haijulikani mara baada ya kudaiwa kutekwa nyara na magaidi wa kundi la Al Shabab, Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa kutoka polisi ya Kenya, huenda madaktari hao wamevushwa hadi nchi jirani ya Somalia. Vikosi vya polisi na jeshi vinaendelea na operesheni ya kuwatafuta madaktari hao.

Madaktari hao ni miongoni mwa kundi la madaktari zaidi ya mia moja kutoa Cuba waliowasili nchini Kenya kwa ombi la serikali, kufanya, kazi kuziba pengo la uhaba wa madaktari nchini humo.

Madaktari hao walitekwa nyara siku ya Ijumaa Aprili 12, Kaskazini Mashariki mwa Kenya, katika Kaunti ya Mandera, karibu na mpaka wa Somalia.

Msemaji wa polisi ya Kenya Charles Owino amebaini kwamba mlinzi wa madaktari hao aliuawa na watekaji nyara, ambao walitoroka na gari na kuingia nchini Somalia. Hata hivyo kwa mujibu wa  Owino akihojiwa na Sauti ya Amerika ya VOA, gari lililokuwa likitumiwa na madakatari hao limepatikana na dereva wake anahojiwa na polisi.