Mexime awapa salamu Simba SC


Kocha mkuu wa timu ya Kagera Sugar, Meck Mexime amesema ana matumaini makubwa ya kuifunga Simba katika mchezo wa ligi kuu utakaochezwa leo katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Mexime amewataka mashabiki wa Wakata Miwa hao kujitokeza kwa wingi uwanjani wakiwa na furaha kwa sababu watashinda na kubaki na alama tatu nyumbani.

Kagera ipo nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 32 hivyo kama watapoteza mbele ya Simba wataendelea kujichimbia kaburi la kushuka daraja.

Mexime amesema anaamini maandalizi aliyowapa wachezaji wake ndio silaha ya kuwafanya kuibuka na ushindi mbele ya mabingwa hao watetezi ambao wapo kwenye kiwango bora kwa sasa. "Mi nawataka mashabiki wa Kagera wajitokeze kwa wingi leo uwanjani maana kila kitu kipo sawa tayari kuhakikisha tunapata ushindi mbele ya Simba na hilo lipo ndani ya uwezo wetu," alisema Mexime.