Viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu,wanaokutana katika mkutano wa kilele wa kila mwaka mjini Tunis, nchini Tunisia wamedhirisha mshikamano wao na kulaani sera za serikali ya rais Donald Trump wa Marekani wanazosema zinaipendelea zaidi Israel.
Hata hivyo viongozi hao hawana msimamo mmoja katika masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na kuirejeshea uwanachama wake muasisi mmojawapo wa jumuia hiyo-Syria.
Mkutano huo wa 30 wa kilele umegubikwa na mada kuhusu vita nchini Syria na Yemen, mzozo wa Libya na ususiwaji wa Qatar na baadhi ya mataifa ya jumuia ya nchi za kiarabu.
Katika ishara za kumaliza mvutano mfalme Salman wa saudi Arabia na Amir wa Qatar, Sheikh Tamin bin Hamad Al Thani waliketi meza moja katika mkutano huo wa kilele hii leo.
Ilikuwa pia mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili kukutana tangu Saudi Araabia ilipotangaza vikwazo dhidi ya Qatar miaka miwili iliyopita.
Amir wa Qatar lakini ameondoka mara baada ya mkutano huo kufunguliwa.
