OCD Njombe aponea tundu la sindano, Atumbuliwa na kurudishwa


Na Amiri kilagalila - Njombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtengua na baadaye kumsamehe mkuu wa polisi wilaya ya Njombe kutokana na mauaji ya watoto yaliyotokea miezi miwili iliyopita mkoani humo.

Rais Magufuli ametoa uamuzi huo mkoani Njombe wakati akizungumza na wananchi katika uwanja wa sabasaba. 
 
“Hata hili suala la mauaji lilitokea hapa halikutakiwa lichukue muda mrefu hivyo, ndio maana RPC wa hapa nimemtoa wala msitafute sababu nyingine nimemtoa kwasababu alishindwa kusimamia hii kazi. Ninataka mambo yawe yanatendeka haraka wewe mtu anapoteza mtoto wa kwanza, anapotea wa pili mpaka wanafika saba haiwezekani na OCD wa hapa bado yupo, na yeye aondoke najua yupo hapa ananilinda, na yeye sio OCD hapa ni lazima watu wawajibike kila maeneo yao watoto saba wanapote mpaka tunaleta polisi wakina Sabas mkoa wa njombe umepata doa kubwa,” amesema Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa endapo yatatokea mauaji hayo kwa mara nyingine mkuu wa mkoa pamoja na viongozi wengine watawajibishwa.

“Siku nyingine yakitokea ya namna hiyo Mkuu wa mkoa unaondoka, DC unaondoka, DAS unaondoka Katibu Tarafa unaondoka mpaka mwenyekiti wa kijiji ikiwezekana na katibu wa CCM wote wanaondoka ili kusudi tufike mahali wote tunachukua hatua mapema. Wakina mama waliopotelewa na watoto wao wameumia lakini nitoe wito kwa ndugu zangu huwezi kutajirika kwa kutoa mtoto,” ameongeza.

Hata hivyo Rais Magufuli aliomba mchungaji yeyote kuongoza Toba kwa mkutano huo huku na yeye mwenyewe akishiriki kwenye toba hiyo na kuamua kumsamehe OCD huyo.

“Asante sana mchungaji kwa toba na huyo OCD nimemsamehe kutokana na maombi haya abaki hapa hapa naomba RPC umwambie nimemsamehe kutokana na maombi haya naomba asitoke mtu mwingine kufanya mabaya na kila mwananjombe akafanye kazi,” amesema Rais Magufuli.

Awali mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka  aliomba radhi kwa niaba ya wananchi huku akimueleza Rais wale wote waliohusika na mauaji ya watoto tayari wamefikishwa mahakamani.

“Mheshimiwa Rais ulinipa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama tumeshirikiana nao na hivyo mimi kwa niaba ya wananchi wote wa mkoa wa Njombe nakuomba radhi kutokana na vifo vya watoto saba bila sababu ya msingi lakini tumesimamia kwa nguvu na wote waliohusika kwa sasa wapo mahakamani,” alisema Olesendeka.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemkabidhi mkuu wa mkoa wa Njombe rambi rambi kiasi cha shilingi milioni 5 kwa ajili ya familia zilizokumbwa na matatizo hayo.