Serikali kutenga maeneo ya ujenzi wa Viwanda mifuko ya karatasi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki, amesema wanatarajia kufanya mazungumzo na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ili kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha mifuko ya karatasi nchini.

Waziri Kairuki alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, katika mkutano wa uwekezaji ulioandaliwa kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Ubalozi wa China nchini.

Kairuki alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko ya karatasi kwa kuanzisha viwanda vya kuitengeneza kupitia mtu mmoja au kwa vikundi.

Kairuki alisema ili kulinda soko la ndani watahakikisha wanaweka makatazo mengi katika uingizaji wa mifuko aina ya karatasi kutoka nje ili kuwapa fursa wazalishaji wa ndani.

“Hii ni fursa kubwa ambayo imejitokeza kwa Watanzania kupitia katazo la serikali la kuzuia matumizi ya mifuko ya kubebea mizigo ya plastiki na tutahakikisha tunaweka makatazo mengi hata ikibidi katika aina ya mifuko kama ya karatasi kutoka nje ili kulinda soko la uzalishaji la ndani,” alisema Kairuki na kuongeza:

“Ombi langu lingine ambalo pia tutazungumza na Tamisemi waone kwamba ni fursa watenge maeneo kwa ajili ya viwanda vya mifuko ya karatasi kuhakikisha kwamba itakapofika Juni Mosi, mwaka huu, maeneo ya uwekezaji yawe yako tayari, lakini pia na taasisi za kifedha ziwe tayari kuwasaidia wawekezaji wa kitanzania ili wawekeze katika furza hiyo muhimu ambayo imejitokeza.”

Alisema inakadiriwa Watanzania wanatumia si chini ya mifuko ya plastiki bilioni tatu kwa kima cha chini na inakadiriwa Mtanzania mmoja kwa wiki anatumia mfuko mmoja mpaka miwili ya plastiki.

“Kwa hiyo kwa fursa hii ambayo imekuja ni kubwa inabidi Watanzania waichangamkie, na tumeambiwa kwamba zipo mashine za kutengeneza mifuko ya karatasi za mpaka Sh. milioni 2,000,000 hadi Sh. milioni 5,000,000, kwa hiyo watu wanaweza kuungana hata kupitia vikundi wakachangamkia fursa hii,” alisema Kairuki.

Pia Kairuki alisema ofisi yake itaendelea kuondoa vikwazo vilivyopo katika sekta ya biashara na uwekezaji nchini.