Serikali ya kiraia kuundwa mara moja Sudan


Mkuu mpya wa baraza la kijeshi mpito nchini Sudan amesema leo kuwa serikali ya kiraia itaundwa baada ya mashauriano na makundi ya upinzani na kuahidi kuwa kipindi cha mpito kitadumu kwa muda usiozidi miaka miwili.

Wakati wa hotuba yake ya kwanza kwa njia ya televisheni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametangaza pia kuondoa marufuku ya kutembea usiku na kuamuru kuachiwa huru kwa watu wote waliofungwa chini ya sheria ya hali ya hatari iliyowekwa na utawala ulioangushwa.

 Wakati huo huo mkuu wa idara ya ulinzi na ujasusi nchini Sudan amejiuzulu leo siku moja baada ya Jenerali Awad Ibn Auf kutangaza kuwachia wadhifa wa kiongozi wa mpito kutokana na shinikizo la waandamanaji.

Salah Abdallah Mohamed Saleh ambaye alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa wakati wa utawala wa rais Bashir amekuwa akituhumiwa kufanya mauaji ya waandamanaji wanaotaka kukomesha utawala wa jeshi kwenye kipindi cha mpito. Shirika la habari la taifa SUNA limeripoti kuwa kiongozi mpya wa mpito Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ameridhia kujiuzulu kwa bwana Salah.