TGDC kuanza uzalishaji Umeme wa Jotoardhi


Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) inatarajia kuzalisha megawati 200 za umeme wa jotoardhi na megawati 500 za joto kwa ajili ya matumizi mengineyo ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza katika mahojiano maalum, mara baada ya  Semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati  na Madini Jijini Dodoma hapo jana,  Meneja Mkuu wa Kampuni ya hiyo Mhandisi Kato Kabaka alisema kuwa dhamira ya Kampuni hiyo ni kuendeleza miradi ya kipaumbele  ili kutimza azma ya uzalishaji uliopangwa kufikia 2025.

 Mhandisi  Kabaka alisema “Tumejipanga kuendeleza miradi ya vipaumbele ya ngozi, Songwe, Luhoi, Kiejo- Mbaka na Natron  ambapo umeme utakaozalishwa utachangia kupunguza gharama za  za uwekezaji  katika viwanda na maeneo ya uzalishaji.”

Akizungumzia baadhi ya  miradi ya  kimkakati  Mhandisi Kabaka alisema kuwa mradi wa Ngozi Mbeya ulioanza mwaka 2015 utakamilika mwaka 2023 ambao upo katika hatua ya uchorongaji wa visima vitatu vya majaribio na  ambavyo vinavyotarajiwa kukamilika ndani ya miezi 23 na kuzalisha  megawati 30.

Alifafanua kuwa umeme wa Jotoardhi ni wa uhakika na endelevu (stable renewable) na unachangia katika usalama wa nishati  (energy security), Jotoardhi ni chanzo kisichoisha na kisichosafirishwa nje ya nchi ikilinganisha na mafuta, mkaa, na gesi.

 Mhandisi Kabaka alisema “Gharama za kuzalisha  umeme wa jotoardhi ni nafuu ikilinganishwa na nishati zinazozalishwa kupitia vyanzo vingine”.

Alibainisha kuwa umeme unaotokana na jotoardhi  unaweza kutumika  maeneo yasiyofikiwa na gridi ya Taifa kwa sababu za kuwa mbali na gridi hiyo.

Aliongeza kuwa nishati hiyo ina faida nyingi na itachangia kuendeleza sekta muhimu katika  uchumi ikiwemo kilimo, ufugaji, utalii,viwanda vidogovidogo na hutumika kama tiba (relaxation and wellness- Balneology).

Aidha, alitaja baadhi ya mikoa yenye rasilimali jotoardhi nchini Tanzania ambayo ni pamoja na; Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Singida, Songwe na Tanga.

Mikakati mingine ya TGDC ni kujenga uwezo wa wataalamu na kupata vifaa vya msingi na kuweka mazingira wezeshi katika uendelezaji wa Jotoardhi.

Umeme wa  Jotoardhi  ni rafiki wa mazingira na haichangii hewa ya ukaa hivyo inasaidia katika utunzaji wa mazingira.