Wadau wa Utalii watakiwa kuhakikisha wanalipa kodi


Na Thabit Hamidu, Zanzibar.

Waziri wa Fedha na Mpango Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa amewataka wadau wa utalii Nchini kuhakikisha wanalipa kodi na kufuata Sheria na Taratibu za Nchi.

Waziri huyo amesema Sekta ya Utalii inamchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi hivyo wadau wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi na kufuata sharia za Nchi.

“Kuna baadhi ya wadau katika sekta hii ya utalii wamekuwa wanafanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu na sheria za nchi ikiwemo kutolipa kodi jambo ambalo linaikosesha taifa mapato na kuzorotesha uchumi wa nchi” alisema Waziri wa Fedha Zanzibar.

Aliyasema hayo jana  wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa wadau wa utalii nchini uliondaliwa na Chama cha watembeza wataliii Zanzibar (ZATO)  na kufanyika katika hoteli ya Madinat Al Bahari Chukwani Mjini Magharib Unguja.

Balozi Ramia alisema Serikali haitamvumilia yeyote ambaye atakiuka sheria za nchi kwa kutolipa kodi zitokanazo na sekta ya utalii.

“Sita kubali uchumi wa nchi uporomokee katika kipindi changu hivyo ntahikikisha mapato yanayotokana na utalii yanakusanywa kwa utaratibu mzuri” alisema Balozi Ramia.

Aliongeza kuwa katika kufuata sharia za Nchi wadau hao watakiwa kuwalipa wafanyakazi wao mishahara inayoendana na utaratibu uliwekwa na   Serikali ya Zanzibar.

“Tulipo tangaza kima cha mwanzo cha mishahara ya Zanzibar katika sekta ya utalii tulipokea malalamiko mengi hivyo nitoe wito kuwa waajiri katika sekta hii muzingatie sheria na taratibu tulizo ziweka katika kuwalipa mishahara na stahiki zao wafanyakazi wenu” aliongeza kusema Waziri Balozi Ramia.

Pia alisema Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza azma yake ya kuimarisha miundombinu iliyo bora katika kutangaza utalii wa Zanzibar na kupata watalii laki tano hadi kufikia mwaka 2020.

“Najua munajua kuwa sekta ya utalii hapa kwetu ina umuhimu kwa kiasi kikubwa ambapo asilimia 27 la pato la taifa linatokana na sekta hii hivyo serikali haina budi kuweka miundombinu mzuri na kutangaza vyema vivutia vya Zanzibar” alieleza Balozi Ramia.

Hata hivyo Balozi Ramia aliwataka wadau hao kutumia mkutano huo kujadili changamoto zinazowakabili ili kupatiwa ufumbuzi na kuinua sekta ya utalii Nchini.

Aidha aliwaambia kuwa wao wanamchango mkubwa katika kukuza Uchumi wa Nchi hivyo mkutano huo uwe njia moja ya kutatua changamoto ambazo zinawakabili sekta sekta hiyo.

Kwa upande wake Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamadi Yusuf Masauni aliwahakikishia wadau wa utalii kuwa hali ya Usalama nchini ipo vizuri na itaendelea kuwa vizuri.

“Mimi nataka kuwambia Hali ya Usalama wa Nchi ipo vizuri kutokana tumejipanga kuhakikisha watalii na wananchi wetu wanaishi katika usalama ambapo jeshi la polisi linaendelea na kazi kubwa ya kuhakikisha usalama unazidi kuimarika Nchini” alisema Mhandisi Msauni.

Nae mwenyekiti wa Chama cha watembeza watalii ZATO Hassani Ali Mzee alisema kuwa lengo la kuandaa mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa utalii na kujadili changamoto zinazowakabili katika sekta hiyo muhimu.

Alisema mkutano huo umehusisha wizara 5 ambapo Nne kutoka serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wizara Moja kutoka Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika Mkutano huo zaidi ya wadau 400 wamejitokeza na kupata fursa ya kujadili mambo mbali mbali katika sekta hiyo ya Utalii.