Wapinzani waongoza uchaguzi katika miji ya Ankara na Istabul


Chama cha rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kinakabiliwa na hatari ya kushindwa katika miji mikubwa ya Ankara na Istanbul, katika uchaguzi wa miji uliofanyika hapo jana. Kulingana na mwenyekiti wa bodi ya juu ya uchaguzi nchini humo Sadi Guven, mgombea wa chama cha upinzani alikuwa anaongoza kwa nafasi ya meya wa mji wa Istanbul huku mpinzani mwingine akiwa tayari ameshinda mjini Ankara.

Rais Erdogan amewataka wafuasi wake kutosikitikia matokeo hayo. "Ningependa kuwaomba hasa kitu kimoja. Msiumizwe au kuvunjwa moyo kwa kusema hamkutarajia matokeo kama hayo. Tunacho chama kilichoshinda asilimia 52 ya kura zote. AKP ndiyo mshindi wa uchaguzi huu. Tunachosema ni twende mbele.

Ndiyo maana tutafakari juu ya makosa yetu, kuyarekebisha na kuendelea na kazi nyingine," alisema Erdogan siku ya Jumapili.

Rais Erdogan, ambaye uwezo wake wa kushinda mfululizo katika uchaguzi ni wa kipekee katika historia ya Uturuki, alionekana kudhoofika safari hii kutokana na mdororo wa kiuchumi uliolikumba taifa hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja, ambapo viwango vya ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei viko juu.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items