Waziri Mkuu Uingereza akiri makubaliano ya Brexit hayatapita Bungeni


Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amekiri kuwa mikakati ya serikali kuidhishwa mpango wake wa Brexit bungeni imefeli, akisema kuna matarajio madogo kwa wabunge kuunga mkono makubaliano yaliokataliwa mara tatu.

Huku Uingereza kwa mara nyingine ikibakisha siku chache tu kutoka tarehe ya mwisho ya kuondoka Umoja wa Ulaya, May aliwashinikiza wabunge wa upinzani kusaidia kupatikana kwa makubaliano ya muafaka.

Baada ya makubaliano ya May na Umoja wa Ulaya kukataliwa kwa mara ya tatu na bunge, waziri mkuu huyo alikialika chama cha upinzani cha Labour wiki hii kujadili mikakati mbadala. Lakini siku tatu za mazungumzo ziliisha bila makubaliano na chama hicho cha Labour kikiishtumu serikali ya kihafidhina ya May kwa kutotoa mabadiliko ya kweli.

Chama cha Labour kinapendelea mchakato laini wa Brexit kuliko ilivyopendekezwa na serikali. Chama hicho kinasema Uingereza inapaswa kubakia ikiongozwa na sheria za Umoja wa Ulaya kuhusu biashara na kuendeleza viwango vya kanda hiyo katika maeneo kama haki za wafanyakazi na ulinzi wa mazingira.