Waziri wa Nishati atoa agizo TANESCO


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaagiza wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchi nzima kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha kuunganisha umeme kwa taasisi zote za umma zilizo katika maeneo yao.

Alitoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya kazi wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma ambapo aliviwashia umeme vijiji vya Buigiri na Mwigamwile.

Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Buigiri pamoja na wananchi, Waziri alisisitiza kwamba kitendo cha kuwasha umeme katika shule hiyo kinalenga kutoa hamasa katika utekelezaji wa maagizo ya serikali kuwa taasisi zote za umma ni lazima zipelekewe umeme.

“Niwaombe viongozi wa Halmashauri za Vijiji na Wilaya nchini kote kuhakikisha taasisi za umma katika maeneo yenu zinalipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu kwa ninyi mlioko vijijini, ili taasisi hizo zote ziunganishiwe umeme,” alisisitiza.

Aidha, kuhusu suala hilo la kulipia gharama za kuunganishiwa umeme, Waziri alilazimika kutoa msisitizo kwa viongozi na wananchi kwani alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watu kulalamika kuwa hawajaunganishiwa umeme lakini baada ya kufuatilia sababu iliyobainika ni kuwa wanakuwa hawajalipia huduma hiyo.

“Lipieni umeme. Msibaki kulalamika tu. Mlalamike mkiwa mmelipia.”alisema Kalemani.

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani aliwataka wanafunzi wa Shule hiyo ya Buigiri kuongeza jitihada katika masomo kwani tayari wamepelekewa umeme ili kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo.

Awali, akizungumza wakati wa tukio hilo la uwashaji umeme, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga alimweleza Waziri kuwa Shule husika imekuwa na kiwango duni cha ufaulu kutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni ukosefu wa umeme tangu ilipoanzishwa mwaka 2007.

Akiwa katika kijiji cha Mwigamwile, Waziri Kalemani aliwasha umeme katika Ofisi mpya ya Serikali ya Kijiji, ili kuendelea kutoa msisitizo wa azma ya serikali kuhakikisha taasisi za umma zinaunganishiwa umeme.