Baba amtoa mwanae auliwe kisa Milioni 5, Polisi wawatia nguvuni


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wawili, Japhet Yahaya Nguku na Andrew Anganile Mwambuluma kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa miaka sita  aitwaye Rose Japhet Mkazi wa Kijiji cha Msewe, Wilayani Mbarali.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya imeeleza kuwa Mei 3 mwaka huu majira ya saa tatu usiku katika Kijiji cha Msewe kilichopo Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya katika msitu wa hifadhi wa Chimala Mtoto aitwaye Rose Japhet alikutwa ameuawa kwa kunyongwa shingo na kukatwa kanyagio la mguu wa kulia ambapo kanyagio la marehemu limekutwa limefukiwa huko Mbalizi, Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Chanzo cha tukio hili ni tamaa ya kupata utajiri ambapo baba mzazi wa marehemu aitwaye Japhet Yahaya Nguku alimtoa mwanae kwa Andrew Anganile Mwambuluma ambaye ni mfanyabiashara kwa malipo ya Tshs 5,000,000 ili auwawe na kisha kukatwa kanyagio la mguu wa kulia na kupatiwa mfanyabiashara huyo ili apeleke kwa mganga ili amtengenezee ndagu (dawa ya utajiri) ili afanikiwe katika biashara zake za Shule anayoimiliki iitwayo HAPPY iliyopo Mbalizi.

Mfanyabiashara huyo Andrew Anganile Mwambuluma amekiri kuhusika na tukio hilo. Ufuatiliaji unaendelea ikiwa ni pamoja na msako mkali wa kumtafuta mganga huyo kwa hatua zaidi za kisheria.