Dereva taksi apandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumteka MO Dewji


Mousa Twaleb mwenye umri wa miaka 46, ambae ni dereva taksi amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kumteka Mfanyabiashara Mohammed Dewji

Amesomewa mashtaka matatu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi likiwemo la kumteka mfanyabiashara huyo mnamo alfajiri ya Oktoba 11, 2018. Kufutia sakata hilo watu 12 walikamatwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na utekaji huo.

Mo alitekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya Oktoba 11, 2018 wakati akifanya mazoezi katika Hoteli ya Colosseum iliyopo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, alipatikana Oktoba 20 katika eneo la Gymkhana baada ya kudaiwa kutelekezwa na watekaji hao.

Familia ya Dewji iliahidi kutoa Sh1 bilioni kwa mtu yeyote ambaye angetoa taarifa ambazo zingesaidia kupatikana kwa kijana wao. Hata hivyo hakuna aliyepata fedha hizo baada ya kupatikana kwake.