Ethiopia yaanza mgao wa umeme


Waziri wa maji na umeme wa Ethiopia Seleshi Bekele amesema, nchi yake imeingia katika mgao wa umeme baada ya kushuka kwa viwango vya maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.

Mgao huo unawagusa watumiaji wa majumbani na viwandani. Kwa mujibu wa waziri Bekele, kupungua kwa kiwango cha maji katika bwawa la Gibe kumesababisha upungufu wa megawati 476 nchini humo.

Kutokana na upungufu huo, Ethiopia imesimamisha uuzaji wa umeme kwa nchi jirani za Djibouti na Sudan, ambao ulikuwa ukiipatia dola milioni 180 za Kimarekani kwa mwaka.

Chini ya mgao wa umeme utakaodumu hadi mwezi Julai, watumiaji wa ndani, watakuwa wakikatiwa umeme kwa masaa kadhaa kila siku, huku makampuni ya kutengeneza saruji na kufua vyuma yakifanya kazi kwa muda mfupi kutokana na mgao huo.