Iran yaituhumu Marekani kwa kuongeza mvutano


Iran imeituhumu Marekani kwa kusababisha hali isiyokubalika ya mvutano na kusema kuwa Serikali mjini Tehran inaendelea kujizuia kwa kiasi kikubwa licha ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa nyuklia na madola mengine yenye nguvu.

Akizungumza leo mjini Tokyo ambako anafanya mazungumzo na maafisa wa Japan Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema kuwa hatua ya Marekani kuongeza mvutano huo haikubaliki.

Matamshi ya Zarif yamekuja saa chache tu baada ya Marekani kuaamuru wafanyakazi wake wasiokuwa na majukumu ya dharura kuondoka katika ubalozi wake wa Baghdad, Iraq kutokana na kile ilichosema kuwa ni kitisho kutoka kwa wanamgambo wa Iraq wanaoungwa mkono na Iran.

Mvutano tayari ulikuwa mkubwa baada ya Rais Donald Trump kujiondoa katika mkataba wa nyuklia mwaka mmoja uliopita, Lakini umeongezeka zaidi katika wiki za karibuni baada ya Marekani kupeleka manowari zake za kivita katika Ghuba ya Uajemi kukabiliana na ilichodai ni vitisho vya Iran.