Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Taifa linakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira kutokana na ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi, hatua inayohitaji mjadala wa kitaifa wa namna ya kukabiliana nayo.
Hayo aliyasema Dar es Salaam katika uzinduzi wa ripoti ya kitaifa ya mazingira iliyoandaliwa na Benki ya Dunia.
Alisema suala hilo ni muhimu kupatiwa mwafaka kwa kuwa inahitajika utatuzi wa changamoto hizo ufanyike bila kuathiri ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi.
“Tanzania ni nchi iliyojaliwa rasilimali za asili ikiwemo misitu, maji, samaki, ardhi ya kutosha na wanyamapori ambazo zinatakiwa kulindwa. Ripoti hii itakuwa ishara ya kutoa wito kwetu sote kuzilinda.
“Kama mjuavyo uchumi wetu kwa kiasi kikubwa unategemea rasilimali za asili na zaidi ya nusu ya watu nchini wanaishi katika maeneo ya vijijini na wanategemea rasilimali hizi kwa chakula, nishati na makazi. Rasilimali za asili ni nguzo ya uchumi wetu na zinasaidia kuimarisha maisha ya watu wetu.
“Kwa kiasi kikubwa uchumi unategemea wanyamapori na kupitia sekta ya utalii taifa limekuwa likinufaika, hivyo ni vyema kuhakikisha vivutio vilivyopo vinatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Samia alisema matumizi ya ardhi pia yanatakiwa kufanyiwa tathmini ya kina na kuwekewa mipaka kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu kwa kuhakikisha sekta zote zinazotegemea matumizi ya ardhi zinarutubishwa bila kuathiri mazingira na uoto wa asili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba, alisema iwapo watu wanaongezeka na kusababisha changamoto kwa fursa zilizopo, kama taifa hatua za kudhibiti rasilimali za asili na mazingira zinatakiwa kuchukuliwa hatua kwa hatua.
