Kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi wa urais Desemba 30, kiongozi wa upinzani nchini DR Congo, Moïse Katumbi Chapwe, amevunja ukimya kuhusu kuendelea kusalia uhamishoni.
Akihojiwa na RFI-France 24, mratibu wa muungano wa upinzani Lamuka ametangaza kwamba baada ya miaka mitatu akiwa uhamishoni, anatarajia kurudi kwa ndege Lubumbashi Mei 20 mwaka huu.
Moise Katumbi ambaye ni mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa jimbo la Katanga, alizuiliwa kuingia nchini DR Congo na kushitakiwa kwa makosa dhidi ya usalama wa taifa. Katumbi mwenye umri wa miaka 53 anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji tangu Mei 2016 baada ya kutofautiana na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila.
Alikuwa anashutumiwa kwa kukodi mamluki na kuwa na pasi ya kusafiria ya Italia, ambapo sheria za Congo haziruhusu mtu kuwa na uraia pacha wa mataifa mawili. Hata hivyo, vyombo vya sheria vya nchini humo vilimsafisha Moise Katumbi kwa makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili katika kesi ya madai ya udanganyifu wa mali.
