Wauguzi wamechoka kukatwa Mishahara, wanataka kujitoa TUGHE na TALGWU



Na John Walter-Manyara

Wauguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara wameomba kujitoa kwenye vyama vya wafanyakazi TALGWU na TUGHE na kujiunga  chama cha wataalamu TANNA ili makato yao kwenye Mishahara yabaki upande mmoja.

Wametoa ombi hilo katika sherehe za maazimisho ya siku ya Uuuguzi duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Dareda Mission ambapo wamesema kuliko kuwa kwenye vyama vingi na kukatwa mishahara kila mahali ni bora waingie kwenye mtandao wa [Check off System].

Wakitoa sababu zaidi za kujitoa katika vyama hivyo wamesema kuwa kuna changamoto  kwani vimekuwa vikichelewesha kutoa maamuzi ya kuwatoa kwenye makato ya ada ya kila mwezi kwenye mishahara yao hivyo wafanye maamuzi kuhusu makato hayo.

Aidha  katika maazimisho hayo wamemweleza Mbunge wa Jimbo la Babati vijijini Jituson kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa nyumba za watumishi kwa baadhi ya vituo hali inayowaletea shida wakati wa usiku,kukosekana kwa uzio na walinzi hivyo kukosa usalama wanapotimiza wajibu wao.

Mbunge wa Babati vijijini Jituson akijibu changamoto hizo amewahakikishia kuwa atazungumza na vyama vyote viwili TALGWU na TUGHE ili kuwaondoa huko kama walivyoomba.

Amewaonya wanasiasa na watu wengine wanaoingilia kazi za  Madaktari na wauguzi waache mara moja kwani wao wanajua wajibu wao hivyo waheshimiwe.

Amewataka wauguzi hao waendelee kutoa elimu kuhusu lishe kwa watoto kwani wengi wamedamaa na kupata utapiamlo kutokana na kukosa lishe bora.

Amesema jambo la kushangaza katika mkoa wa Manyara asilia 36 ya watoto wana utapiamlo na udumavu ilhali mkoa umejaliwa kuwa na vyakula vyenye uwezo wa kutoa lishe bora kwa mtoto.

Mbunge huyo pia ametembelea na kuwafariji wagonjwa katika wodi zote katika Hospitali ya Dareda na kuwapa zawadi mbalimbali.

Naye Mganga mkuu wa wilaya ya Babati Dr.Madama Hosea amewapongeza wauguzi  kwa kazi kubwa wanayofanya kuhudumia wagonjwa akiwasisitiza kutumia lugha nzuri wawapo kazini.

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka ifikapo Mei 12, ambapo wauguzi  kwa mwaka huu wanasisitiza kauli mbiu yenye ujumbe usemao “WAUGUZI SAUTI INAYOONGOZA AFYA KWA WOTE.”