Amuua mpenzi wake kisha kujiteketeza kwa moto



Na James Timber, Mwanza

Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Fungo Mayala (34) kabila Msukuma, Mfanyabiashara wa samaki Mkazi wa Mhandu Kisiwani wilayani Nyamagana jijini Mwanza amemshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili mpenzi wake na kumkaba hadi kufa Hamida Joseph (30) kabila Muha Mjasiliamali na Mkazi wa jijini hapa.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Muliro Muliro amesema kuwa tukio hilo limetokea Juni 18, mwaka huu Majira ya 16:00, baada ya mgogoro wa kimapenzi wa muda mrefu kati ya marehemu na mtuhumiwa ambapo marehemu alimripoti mtuhumiwa polisi kisha kukamatwa na kufikishwa mahakamani mnamo Juni 11, Mwaka huu.

ACP Muliro alisema kuwa Juni 18, mwaka huu siku ambayo kesi ilipangwa kusikilizwa marehemu alikwenda mahakamani kuomba kumsamehe mshtakiwa huyo, mahakama iliridhia ombi hilo na kuondoa kesi hiyo mahakamani.

Kamanda alieleza baada ya msamaha huo mtuhumiwa alikwenda nyumbani kwa marehemu na kuingia ndani kisha alifunga mlango na kuanza kumpiga marehemu ndipo majirani walisikia kelele za marehemu akiomba msaada lakini walishindwa kufungua mlango ndipo walitoa taarifa polisi.

Alisema polisi walifika eneo la tukio na kukuta nyumba yote ikiwa inafuka moshi na kushirikiana na majirani kuvunja mlango na kumkuta marehemu akiwa tayari amefariki dunia huku moto ukiwa umemuunguzwa sehemu mbalimbali ya mwili wake.

Pia kamanda alisema mtuhumiwa alikutwa mahututi kutokana na majeraha ya moto na kukosa hewa kutokana moshi, polisi walimchukua kumpeleka hospitali lakini alifariki dunia wakiwa njiani.

Aidha miili ya marehemu wote wawili imehifadhiwa Hospitali ya Mkoa Sekou Toure kwa ajili ya uchunguzi wa daktari, pindi uchunguzi utakapokamilika itakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia