Baba kunyongwa kwa kuua watoto wake, licha ya mama kumsamehe

Baba aliyewaua watoto zake watano nchini Marekani amehukumiwa kunyongwa mpaka kufa, mahakama imeamua na kutupilia mbali ombi la msamaha la mama wa watoto hao.

Mama wa watoto hao Amber Kyzer, aliiambia mahakama siku ya Jumanne kuwa, baba huyo Tim Jones Jr, 37 ambaye alishakutwa na hatia ya mauaji, "Hakuonesha huruma hata kidogo kwa watoto. Kama ningeweza ningemrarua uso wake hata sasa... lakini watoto wangu walimpenda."

Hukumu hiyo imetolewa baada ya waendesha mashtaka kudai kuwa, hukumu ya kifungo cha maisha jela itakuwa ni sawa na "kumpeleka Timmy chumbani kwake."

Jimbo la South Carolina halijanyonga mfungwa toka mwaka 2011.

Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ambayo ilimtia hatiani bwana huyo kwa mauaji ya watoto hao waliokuwa na mwaka mmoja mpaka miaka minane mwaka 2014.

Wazee wa baraza wa mahakama hiyo, wanaume saba na wanawake watano walitakiwa kufikia uamuzi wa pamoja, na laiti wangetofautana Jones angehukumiwa kifubgo cha maisha jela.

Wazee hao wa baraza walikubaliana kuhusu hukumu hiyo baada ya saa mbili za majadiliano.

Katika mijadala ya kisheria juu ya hukumu hiyo, waendesha mashtaka waliwataka wazee wa baraza kukumbuka ni kwa namna gani bwana huyo aliwaua watoto.

Jones alikiri kuwa alimfanyisha mazoezi magumu mtoto wake mkubwa mpaka akadondoka na kufariki.

Baada ya hapo aliwanyonga wanne waliosalia mmoja baada ya mmoja, na kupakia miili yao kwenye gari na kuliendesha kwa siku tisa, kabla ya kuitupa kwenye matanki ya takataka kwenye jimbo la Alabama.

Katika mwenendo wa kesi, baba wa Jones, mama yake wa kambo, dada na kaka zake wawili wote walipanda kizimbani kumuombea apewe adhabu ya kifungo cha maisha.

Baba wa Jones alivua shati lake mbele ya mahakama na kuonesha michoro ya tatoo ya wajukuu zake hao ambao wameuawa na baba yao.

Mama wa watoto hao alisema kuwa anaomba asinyongwe kwa niaba ya watoto wake.

Bi Kayzer alimuombea msamaha.

"Watoto walimpenda, na endapo nitaongea kwa niaba yao, basi kitu pekee nitakachosema ni kumuombea msamaha."