Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka taasisi ya Al – Hikma Foundation kuzingatia kiwango chenye uwiano kwa washiriki wa Zanzibar, pale inapoandaa mashindano ya kuhifadhisha Qur-ani.
Alhaj Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa taasisi ya Al-Hikma Foundation kutoka Jijini Dar es Salaam, uliofika kujitambulisha pamoja na kumuombea dua ya kumtakia maisha mema na uongozi bora.
Alhaj Dk. Shein alisema kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi hiyo pale inapofanya shughuli zake, hususan zinazoambatana na mashindano ya kuhifadhi Qur-ani pamoja na upatikanaji wa fursa mbali mbali zikiwemo za kijamii, kuzingatia umuhimu wa kuongeza kiwango cha kuishirikisha Zanzibar kwani kiwango cha sasa ni kidogo.
Alisema amevutiwa sana na juhudi zinazofanywa na Taasisi hiyo na kubainisha mafanikio yaliofikiwa kuwa ni matunda yanayotokana na kuwepo kwa viongozi bora, sambamba na kuitaka kuendelea kuitumia kikamilifu fursa ya kuwa na mlezi mahiri Alhadj Ali Hassan Mwinyi.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alisema usimamizi wa mashindano ya kuhifadhisha Qur-an kunakofanywa na taasisi hiyo ni njia bora katika kuwajenga watoto kupenda kuhifadhi qur-an, akibainisha umuhimu wa jambo hilo kwa msingi kuwa ni lazima Qur-an ihifadhiwe na kuendelezwa.
Alisema Zanzibar ina historia ya kuwa chemchem ya dini ya kiislamu na kueleza kuwa kwa nyakati tofauti imefanikiwa kutowa wanazuoni mashuhuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo akatowa wito kwa watu mbali mbali kuja kujifunza masuala ya dini ya kiislamu.
Alhaj Dk. Shein aliipongeza taasisi hiyo kwa kufikisha miaka 22 tangu kuanzishwa kwake, sambamba na kutekeleza jukumu lake la kusimamia mashindano ya Qur-an kwa kipindi chote hicho.