Marekani yakiri ndege yake kudunguliwa na Iran

Jeshi la Marekani limethibitisha ripoti za kudunguliwa kwa ndege yake isiyo na rubani lakini likasema kuwa tukio hilo limetokea kwenye anga ya kimataifa.

Taarifa hizo zinakinzana na ripoti za awali zilizotolewa na Iran kuwa ndege hiyo ya Marekani ilidunguliwa kwasababu ilikiuka masharti kwa kuruka katika anga yake.

 Msemaji wa kamandi kuu ya jeshi la Marekani, Kapteni Bill Urban, ameziita ripoti za Iran kuwa za uongo, na kwamba hilo halikuwa shambulio la kiuchukozi katika ndege yake.

Amesema udunguaji huo umetokea katika anga ya kimataifa juu ya mlango bahari wa Hormuz, siku ya Jumatano.

Tukio hilo linakuja wakati ambao mvutano baina ya Iran na Marekani unazidi kuongezeka kufuatia mashambulizi ya meli katika Ghuba ya Uajemi.

Marekani inaituhumu Iran kufanya mashambulizi hayo. Iran yenyewe imekana kuhusika kwa namna yoyote.