Mtoto wa darasa la nne afariki kwa ajali ya Maji


Na Ahmad Mmow, Lindi 

Mwanafunzi wa shule ya msingi Mtanda, katika Manispaa ya Lindi, Shaban Ramadhan(12) amekufa kwa maji katika bahari ya Hindi,manispaa ya Lindi.

Akizungumzia tu hilo la kuhuzunisha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Pudensiana Protas alisema mtoto huyo alikufa juzi majira ya saa kumi alasiri baada ya maji kumzidi nguvu alipojaribu kuogelea katika bahari ya Hindi jirani na hoteli ya Chamikumbi.

Kamanda Protas alisema mtoto huyo akiwa na wenzake wawili walitoka nyumbani kwao katika
mtaa wa Mtanda na kwenda baharini. Ambako mtoto huyo alijitosa majini.

 ''Inaelekea alikwa anajaribu kuogela, lakini maji yalizidi nguvu akazama,'' alisema afande Protas.

Kamanda huyo alisema  juhudi za kutafuta mwili wa Shaban zilizaa matunda. Kwani ulipatikana na kutambuliwa na ndugu na jamaa zake.

Alirudia kutoa wito kwa wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao ili kujua maeneo wanayopendelea kwenda na kucheza ili wawatahadharishe maeneo hatarishi yasiyofaa kwenda na kucheza.

Hilo nitukio la pili kutokea ndani ya wiki hii. Kwani siku mbili zilizopita, jirani na kituo cha mabasi cha Lindi, alikutwa mtoto kwenye karo ya choo akiwa amekufa.