Mtaalamu maalum wa kisheria wa Umoja wa Mataifa anayechunguza mauaji ya mwandishi habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi, amependekeza ufanyike uchunguzi juu ya uwezekano wa ushiriki wa mwanamfalme Mohammed bin Salman katika mauaji hayo, akisema upo ushahidi wa kuaminika kumhusisha mrithi huyo wa ufalme na mauaji hayo.
Madai kuhusu uwezekano wa jukumu la moja kwa moja la mrithi wa kiti cha ufalme Mohammed bin Salman katika mauaji ya Khashoggi Oktoba mwaka uliopita, yamebainishwa kwa kina katika ripoti mpya ya mchunguzi maalumu kuhusu mauaji ya kinyume cha sheria, Agnes Callamard.
Ripoti hiyo yanye kurasa 101 juu ya mauaji ya Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki, inatoa mwito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa au Katibu Mkuu Antonio Guterres, kufungua uchunguzi zaidi wa uhalifu.
