Mwenge wa Uhuru Babati wazindua Nyumba ya kisasa ya Mkulima wa Pareto



Na John Walter-Babati

Mwenge wa uhuru ukiwa wilaya ya Babati vijijini mkoani Manyara, umezindua nyumba ya kisasa yenye thamani ya shilingi Milioni 40 iliyojengwa na mkulima wa kijiji cha Mandagew- Bashnet, Hando Wema kutokana na zao la Pareto.

Akizungumza na Muungwana Blog,Wema amesema ameanza kufanya kilimo cha zao hilo tangu mwaka 2017 kijijini hapo.


Ndugu wa Hando Wema,Samweli Wema anaomba serikali iwafikishie huduma ya umeme ili waweze kukausha Pareto kuliko kutumia kuni ambazo hupatikanaji wake ni mgumu.

“Sasa tunaomba serikali itupatie umeme wa Rea kama kuna uwezekano ili tuweze kukausha  kwa urahisi kwani kwa sasa inatubidi tukate miti ili kupata kuni za kukaushia,kwa kweli  serikali ituangalie kwani tukipata umeme wengi wataanza kufanya kilimo cha Pareto’alisema Bwana Samweli

Bwana shamba ambaye pia ni msimamizi wa zao la Pareto kwa kanda ya Kaskazini  Goodluck Tairo, anawashauri wananchi kulima zao la Pareto kama zao la biashara kwa kuwa  lina manufaa  makubwa tofauti na mazao mengine.

“Naomba niwashauri kuwa mahindi ni zao la chakula lakini ni vizuri kulima Pareto kama zao la Biashara kwani pesa yake ni ya hapa na hapa kila mwezi na halishambuliwi na magonjwa kama mazao mengine’alisisitiza Tairo.


Mtaalamu huyo anasema, zao la Pareto lenye sifa ya kuvumilia ukame lina uwezo wa kuvunwa kila baada ya wiki mbili  ndani ya mwaka mzima  tofauti na mazao mengine ambayo msimu wake huwa mmoja.

Akiifungua nyumba hiyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mzee Mkongea Ali amempongeza mkulima kwa juhudi alizozionyesha na kuwasihi wakulima wengine kulima mazao ambayo yana tija kwao.

Kumbuka kuwa zao la Korosho huvunwa maua yake ambayo hutumika kwa ajili ya kutengenezea viuatilifu mmbalimbali vinavyotumika kuua wadudu waharibifu au wenye kuleta hatari ya magonjwa kama vile Mbu aenezae Malaria.