Namna utakavyoweza kudumisha uhusiano na mwenza wako


Hakuna raha katika ulimwengu huu kama kumpata mpenzi mwenye kujali na kuonesha hisia za kweli kwako, hii itakufanya dunia hii uione ni ya kwenu wawili tu hii ni kwa sababu wote mnapendana. Hivyo kama umepata mpenzi ambaye mnapendana ili muweze kudumisha mahusiano yenu unatakatiwa kufanya mambo yafuatayo;

Onyesha Upendo Wako
Kila mtu ana namna yake tofauti ya kuonyesha upendo, lakini vyovyote itavyokuwa ni jambo la muhimu sana kuonyesha hisia zako kwa mpenzi wako. Mara nyingi wapenzi wa muda mrefu wanasahau juu ya hili.

Maneno kama “Nakupenda”au majina ya mahaba kama “Mpenzi” au ”La-azizi” yanachangia sana kuonyesha mapenzi na kumfanya mwenza wako kujisikia vizuri. Maneno haya yanaposemwa kwa hisia halisi na toka moyoni yana mchango mkubwa katika kuboresha mahusiano.

Mawasiliano

Mawasiliano ni muhimu sana baina ya wapenzi.
Hata kama umebanwa na kazi pata dakika chache za kuongea na mpezi wako na kumtaka hali. Andika hata ujumbe wa maneno au barua pepe. Mwambie mpenzi wako ulipo kila mara inapobidi ili kumjengea imani na wewe na kumpa amani moyoni. Tuma ramani ya mahali ulipo kama unatumia simu ya “Smart” (Tuma location kwenye whatsapp)

Mawasiliano ni ufunguo wa kudumisha upendo.
Wakati kuwasiliana na mpendwa wako, kumbuka kwamba upendo ni muhimu. Ongea toka moyoni na si kwa ajili ya kutimiza wajibu tu, kwani mpenzi wako atajua tu kama hakuna mahaba katika mawasiliano yenu hivyo kutoleta faida ile inayotegemewa.

Mawasiliano mengine ni yale ya kuelezana yaliyo moyoni. Mweleze mwenza wako linalokusibu ili kupata ufumbuzi wa pamoja. Wapenzi wanaoongea kwa utulivu siku zote watakuwa pamoja.

Zawadi
Tafuta kitu cha kumpa mpenzi wako. Si lazima kiwe na thamani kubwa. Inaweza ikawa pipi au matunda tu. Mnunulie zawadi kila inapowezekana hasa unaposafiri au katika siku yake ya kuzaliwa, hii itamfanya akuone wewe ni thamani pia ni wa maana sana kwa sabau miongoni mwa umuhimu wa zawadi kwa yule umpendaye ni kwamba atamfanya mtu huyo ajisikie yeye ni wa pekee pia ni wa thamani sana kwako.