Njia za uwakika zitakazokusaidia kufikia kwenye utajiri


Fedha ni muhimu sana kwenye maisha yetu ya kila siku. Hii ni kwa sababu fedha ndio inatuwezesha kupata mahitaji yote ya msingi kwenye maisha.

Hivyo ili kuwa na maisha bora ni muhimu sana kuwa na fedha za kutosha. Kwa kifupi inabidi uwe na fedha za kukutosheleza au kwa kutumia neno rahisi ni muhimu wewe kuwa tajiri. Au kama hupendi kutumia neno tajiri kwa kufikiri sio neno zuri basi ni muhimu wewe kuwa na uhuru wa kifedha.

Utakuwa na uhuru wa kifedha pale ambapo fedha inakuwa sio hofu tena kwako. Na ili kuweza kufikia hatua hii kuna njia ambazo ni muhimu kupitia. Leo tutajadili njia nne za uhakika za kufikia utajiri na jinsi unavyoweza kuzitumia. Kwa bahati mbaya sana katika njia hizi ile ambayo inapendwa na watu wengi haipo. Njia hiyo inayopendwa na watu wengi na ambayo haiwezi kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha au utajiri ni ajira.

Zifuatazo ni njia nne za uhakika za kufikia utajiri.

Biashara.
Hii ni njia ya kwanza ya uhakika ya kufikia uhuru wa kifedha. Katika biashara unaweza kutengeneza au kutafuta soko la bidhaa, huduma au hata mawazo yanayoweza kuboresha kitu. Biashara inakuwezesha wewe kutumia nyenzo ya muda wa watu wengine, fedha za watu wengine na hata utaalamu wa watu wengine kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Aina ya biashara tunayozungumzia hapa ni biashara kubwa ambayo haikuhitaji wewe kila mara ndio iweze kwenda vizuri.

Kama bado hujaingia kwenye biashara anza sasa mchakato wa kuangalia ni biashara gani unayoweza kufanya. Kabla hujaingia kwenye biashara yoyote hakikisha inauwezo wa kukua na kuendeshwa bila ya wewe kuwepo moja kwa moja.

Uwekezaji.
Hii ni njia nyingine muhimu ya kuweza kujitengenezea kiasi kikubwa cha fedha na hivyo kufikia uhuru wa kifedha. Katika uwekezaji unaweza kuwekeza fedha zako katika hisa, vipande na hata mifumo mingine ya uwekezaji wa fedha. Uzuri wa uwekezaji ni kwamba wewe unawekeza tu fedha zako na kuwa mfuatiliaji, huhitaji kufanya kazi moja kwa moja, bali fedha yako ndio inakufanyia kazi.

Kila mtu anaweza kuwa muwekezaji mzuri kama atapata elimu husika juu ya uwekezaji. Kama hujui uanzie wapi tembelea UWEKEZAJI TANZANIA ili uweze kujifunza mambo muhimu kuhusu uwekezaji.

Umiliki wa mali.
Njia nyingine unayoweza kuitumia kufikia utajiri ni umiliki wa mali. Unaweza kununua ardhi na kukaa nayo na jinsi siku zinavyokwenda thamani yake inaongezeka. Pia unaweza kujenga nyumba kwa ajili ya biashara yaani kuuza au kupangisha. Kwa njia hizi unatumia mali unazomiliki kutengeneza fedha zaidi.

Intaneti.
Najua unaweza kushangaa intaneti inawezaje kukufanya wewe kuwa tajiri. Ukweli ni kwamba intaneti imetengeneza matajiri wengi sana na hata wewe unaweza kuwa mmoja wao. Intaneti ina njia nyingi sana unazoweza kuzitumia kutengeneza fedha. Unaweza kutangaza biashara zako mwenyewe, unaweza kuanzisha blog au website yenye kutoa taarifa muhimu na kutengeneza wafuasi ambao unaweza kuwatangazia biashara za watu wengine na ukalipwa fedha nyingi.

Uzuri wa intaneti hasa huku kwenye nchi zetu za kiafrika bado ni changa sana na hivyo kuna nafasi kubwa ya kuweza kunufaika. Na pia intaneti ni nzuri sana kwa sababu mtu yeyote mwenye juhudi na maarifa hata kama hana mtaji kabiasha anaweza kuanza kutengeneza fedha kupitia intaneti.

Angalizo muhimu kwa njia hizi nne.
Sio kwamba ukishaingia tu kwenye moja ya njia hizi nne basi tayari wewe ni tajiri. Unahitaji kufanya kazi kwa bidii na maarifa na pia unahitaji uvumilivu mkubwa kwa sababu changamoto ni nyingi sana na zinaweza kukukatisha tamaa.

Pia jinsi unavyoanza mapema ndio unavyojiwekea nafasi nzuri ya kufikia utajiri mapema. Mtu anayeanza biashara au uwekezaji akiwa na miaka 30 ni tofauti kabisa na mtu anayeanza akiwa na miaka 40 au 50. Jitahidi uanze sasa bila ya kujali umri ulionao.

Muhimu zaidi ni kwamba unaweza kuzitumia njia zote. Sio kwamba ukishatumia njia moja basi nyingine huruhusiwi, hapana, unaweza kutumia zote unavyotaka mwenyewe. Kwa mfano unaweza kuwa na biashara ambayo pia umeiweka kwenye mtandao na faida unayopata kwenye biashara zako unaiwekeza kwenye biashara hiyo na kwenye aina nyingine za uwekezaji na pia unanunua mali zaidi.