Umeme vijijini 27,000 tu - Waziri Kalemani


Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amerudia agizo la serikali lililotolewa Mei Mosi, mwaka huu na kusisitiza kuwa hakuna mwananchi wa kijijini atakayeunganishiwa umeme kwa gharama ya zaidi ya Sh 27,000.

Ametoa msisitizo huo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (CCM) aliyetaka kujua pamoja na tamko hilo la serikali, Tanesco bado wanaunganishia watu umeme kwa zaidi ya Sh 27,000.

Dk Kalemani alisema kila mwananchi wa kijijini anatakiwa kuunganishiwa umeme kwa Sh. 27,000 kwa kampuni yoyote inayounganisha umeme kama ni Tanesco, REA au mkandarasi mwingine yoyote.

Alisema hayo ndiyo maagizo ya serikali na kila mkandarasi anatakiwa kutekeleza agizo hilo, kwa kuwaunganishia umeme wananchi waliopo vijijini kwa gharama hiyo na si zaidi.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava (CCM) aliyetaka kujua ni lini usambazaji wa umeme kupitia REA utakamilika katika vijiji vya jimbo la Korogwe Vijijini, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alisema serikali inaendelea na kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vyote.

Naibu Waziri Mgalu alisema serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini hadi Juni, 2021.


Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items