Wadau wa Lishe waapa kutokomeza udumavu na utapiamlo Kagera



Na Clavery Christian Bukoba.

Katika kikao cha kamati ya wadau wa Lishe mkoani kagera wamesema kuwa Taifa bila kuwa na watu wenye lishe bora litaangamia na kuwa na kizazi kisichoweza kufanya kazi vizuri.

Wamesema kuwa lishe inaanzia pale mama anapokuwa mjamzito ambapo mama akiwa na mimba akapata lishe nzuri atajifungua mtoto mwenye Afya nzuri tofauti na mama anayekosa lishe akiwa mjamzito kitu ambacho kinaweza kumpelekea kujifungua mtoto njiti au ambaye anamapungufu ya viungo.

Aidha wamesema kuwa ni muhimu sana baba kuanza kucheza na mtoto akiwa bado tumboni na kuhakikisha anamuhudumia mama vizuri kipindi chote cha ujauzito na kuhakikisha mama anapata lishe bora.

Wakieleza vipaumbele vyao kwa sasa katika kuboresha lishe mkoani kagera wamesema kuwa watahakikisha wanatoa Elimu kwa vijana kuhusu lishe bora na kwa mama na mtoto, kuhamasisha jamii ulaji wa vyakula vinavyokidhi mahitaji ya lishe bora, kuanzisha na kuboresha huduma kwa wagonjwa wa utapiamlo na kuboresha huduma ya kudhibiti magonjwa yasiyo ambukiza, kama vile presha, kisukari n.k.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa kikao hicho ambaye ni Katibu tawala wa mkoa kagera Prof Faustini Kamzola ameyata mashirika hayo kutumia vyombo vya habari hususani radio zilizoko mkoani humo kutoa Elimu ya lishe kwa jamii na kutafuta makampuni ya mitandao ya cm kudhamini vipindi hivyo ili waweze kutoa Elimu kwa jamii kiuraisi na haraka zaidi kwani hali ya udumavu mkoani humo haridhishi kabisa.

Kikao hicho kimejumuhisha taasisi nne zisizo za kiserikali ambazo ni Agri Thamani Foundation, Word Vision, USAID Boresha Afya na IMA Word Health viongozi wengine walioudhuria ni mganga mkuu wa mkoa, afisa afya mkoa, afisa Maendeleo ya jamii mkoa na afisa uchumi mkoa pamoja na viongozi wa dini.