Na Amiri kilagalila-Njombe
Wananchi wa kijiji cha Lupalilo wilayani Makete mkoani Njombe wamemtaka afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw. Katiba Mgaya kuacha tabia ya kuondoka kijijini hapo na kufanya shuguli za kijiji hicho akiwa kijiji jirani na kusababisha kukwama kwa baadhi ya shughuli za maendeleo.
Katika ajenda ya wananchi hao waliomba iingizwe kwenye ajenda za mkutano wa hadhara wa kijiji hicho uliofanyika Juni 6 kijijini hapo, wananchi hao walisema wakati mwingine kuondoka kwake kunasababisha baadhi ya shughuli za maendeleo kukwama hasa zile zinazohitaji utatuzi wa Afisa mtendaji huyo
Wananchi hao wamesema shughuli za ujenzi wa shule ya msingi Lupalilo zimesimama kutokana na fedha za michango kutowasilishwa shuleni licha ya wao kuazimia ziwasilishwe kwa mwalimu mkuu, hivyo kumtaka Mtendaji huyo kuzitoa fedha hizo kwenye mkutano huo ili zipelekwe kwenye shughuli za ujenzi
“kwa kuwa mwalimu mkuu kuchukua fedha kwa mtendaji ameshindwa,sasa tulikuwa tunaomba mtendaji akabidhi fedha hizo mbele ya wananchi kwa kuwa shughuli pale zinasimama,na siment za wadau pale zinaganda jamani tuamke tuwe wakweli, tuchukue hizo fedha kabla hatujaenda kwenye wod,na serikali ituambie kwanini fedha hizo hazipelekwi mimi Napata aibu kwa wenzangu wanaoishi nje ya makete”alisema Supa sanga mmoja wa wananchi
Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Method Pela amesema kutokana na suala hilo amekuwa akipata wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yake hivyo kutishia kujiudhuru mbele ya mkutano huo
“kwa kweli wananchi mimi mpaka sasa nafikia sehemu ya kuacha kazi siwezi”alisema mwenyekiti
Afisa Mtendaji huyo wa kijiji Bw. Katiba Mgaya ametolea ufafanuzi wa suala hilo kwa kusema yeye hausiki na ujenzi wa majengo hayo bali jukumu lake ni kukusanya michango kama walivyokubaliana
“kwa ujumla mwalimu mkuu ndio anatakiwa afike kwenye ofisi ya kijiji akabidhiwe michango ya shule tayali kwa kuendeleza shughuli zake za pale shuleni,sasa hapa inageuzwa mimi nataka kuingia kwenye manunuzi hii sio sawa,labda kwa majibu hayo mwalimu mkuu hajaja kuchukua fedha kwangu, na kuniambia kwamba tunataka huu mkutano uthibitishe kukabidhi fedha mimi sina shida mkitaka nawapa shida haipo, tusifike mahala tukalaumiana vitu ambavyo vipo wazi”alisema mtendaji.
Aidha Baada ya majadiliano ya muda mrefu afisa Mtendaji huyo akakiri makosa yake mbele ya mkutano huo na kuomba radhi kwa wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na kukabidhi shilingi 320,000/- kwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lupaloli mbele ya mkutano huo
“jamani hela hii hapa laki tatu na elfu 20 ninaomba nimsainishe mwalimu kwamba anakiri kupokea,lakini samahani najua shughuli imesima kwa sehemu kubwa, lakini hata kama mimi nitaonekana nimesimamisha maendeleo bali itaonekana katiba ndio imesababisha”alimaliza kusema afisa mtendaji