Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema Watanzania tisa wameuawa baada ya kupigwa risasi na wengine kushambuliwa kwa mapanga na watu wanaodaiwa kuvalia sare za jeshi katika kijiji cha Mtole kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji pembezoni wa Mto Ruvuma.
Tukio hilo lilitokea Juni 26 mwaka huu ambapo mbali na mauaji hayo, lakini pia vibanda zadi ya 30 vilichomwa moto na watu wengine nane kujeruhiwa wakiwemo Watanzanii sita na raia wa Msumbiji wawili wakati wanawake wawili na mtoto mmoja walichukuliwa kwa nguvu na waliofanya tukio hilo bado hawajajulikana walipo.
Hali hiyo ilimlazimu IGP kuwasili mkoani Mtwara kwa ajili ya kubaini chanzo cha mauaji hayo na kisha kutuma salamu kwa waliofanya uhalifu huo na kwamba wale wote waliofanya tukio hilo kwa kushirikiana na serikali ya Msumbiji watahakikisha wanatafutwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Naomba niseme tu sisi tuko vizuri kwa kuhakikisha hali ya usalama mkoani hapa na maeneo mengine hapa nchini yanakuwa shwari lakini pia kijiji kile ambacho tukio limetokea na kule ambako marehemu wamezikwa tutaimarisha ulinzi wa kutosha hadi hapo hali itapokuwa imetulia," alisema Sirro.
"Kumuua Mtanzania, narudia ukimuuwa Mtanzania ujue na wewe hauko salama popote ulipo na wengine watanisikia, hauko salama au utafia huko huko ulipo au utarudishwa Tanzania na wewe uijue dunia ilivyo,"alisema IGP Sirro.
Sirro alisema hawatakuwa na muhali juu ya hilo kwa waliohusika na tukio hilo kwa serikali inahakikisha Watanzania wote wanaishi kwa amani na utulivu.
"Uwezo mkubwa tunao, tutatumia Intapol na tutatumia sheria zilizopo kuhakikisha waliofanya mauaji kwa Watanzania wetu wanapatikana wakiwa salama au wakiwa wametangulia mbele ya haki," alisema.
