Wazazi wahamasisha utoro kwa watoto wao

Baadhi ya wazazi na walezi katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambao hawakutaka watoto wao waende shule wamekuwa wakihamasisha utoro kwa watoto wao, ili itakapotimia idadi ya siku 90 basi mtoto afutwe shuleni.

Hayo yalisemwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai wakati akisoma risala kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika shule ya Wasioona ya Buigiri.

Alisema kumekuwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya wazazi na walezi kuhamasisha utoro kwa watoto wao ili itakapotimia idadi ya siku 90 basi mtoto afutwe shuleni.

Pia alisema jamii imekuwa haiwajibiki katika makuzi na malezi ya watoto huku wazazi na walezi wakiwaachia walimu na mitandao ya kijamii na runinga jukumu la kulea watoto.

"Hali hiyo imesababisha kuwapo na mmomonyoko wa maadili na ongezoko la mimba za utotoni hasa kwa shule za msingi,"alisema.

Alisema takwimu zinaonesha katika kipindi cha miaka mitatu mwaka 2017 kulikuwa na mimba 36, mwaka 2018 mimba 24 na hadi kufikia Mei 20, mwaka huu kulikuwa na mimba sita.

Alisema mimba hizo taarifa zake zilipelekwa polisi lakini wazazi wa mabinti wanaopata mimba wamekuwa hawatoi ushirikiano katika kuhakikisha mtuhumiwa anachukuliwa hatua za kisheria.

"Baadhi ya wazazi huwashawishi wanafunzi wasifanye vyema kwenye mitihani yao na kuwaozesha au kuwapeleka kufanya kazi za ndani"alisema na kuongeza kuwa, Mwaka 2016 shule ya Mapinduzi haikufaulisha hata mwanafunzi mmoja, si kwamba wanafunzi hawana uelewa bali wazazi na walezi wamefanikiwa kuwarubuni watoto wao ili kuandika majibu yasiyo sahihi ambayo yalisababisha wasifaulu na mwaka 2017 alifaulu mwanafunzi mmoja."