CCM Dodoma yajinasibu kushinda kwa kishindo uchaguzi Serikali za Mitaa


Na Enock Magali, Dodoma

Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika mapema mwezi Septemba mwaka huu,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Antony Mavunde,ametoa vifaa vya uenezi (Spika na visemeo) pamoja na Bendera za chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kila kata pamoja na uongozi wa wilaya wa Jumuiya kwa ajili ya kurahisisha shughuli za uchaguzi huo.


Mavunde ametoa na kukabidhi vifaa hivyo hii leo katika ukumbi wa CCM Makao Makuu Jijini Dodoma,ambapo amesema lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Seriklai za Mitaa unaendeshwa kisayansi pasi na changamoto zozot, na pia vifaa hivyo ametoa kwa lengo la kutimiza ahadi yake aliyoitoa mwaka 2017.

"Mwaka 2017 nilitoa ahadi ya kuhakikisha kuwa kila kata katika jimbo langu wanapata visemeo vitakavyowasaidia kuendeshea mikutano yao ya ndani na nje,na hii ni kutokana na changamoto iliyopo huko kwenye kata,mmekuwa mkiingia kwenye gharama za kukodi vifaa na kadhalika,lakini mimi nimekuwa nikivinunua kidogo kidogo na hatimaye leo vimekamilika,"Alisema.

Aidha Katika kipindi chake cha miaka mitatu ya ubunge Mavunde amesema,tayari amekwisha tatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa jimbo lake ikiwemo masuala ya ukosefu wa Maji,Umeme,Migogoro ya Ardhi na huduma nyingine za kijamii.

"Katika miaka yangu mitatu ya uongozi nimejitahidi sana kuhakikisha natatua changamoto za wananchi,mapungufu yaliyopo ni ya kiubinadamu tu,kwa kushirikiana na wenzangu tumeweza kutatua changamoto mbalimbali za wananchi,sasa hivi najisikia furaha sana kwani wananchi wameonyesha Imani kubwa na Chama"Aliongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Dodoma Mjini ambaye pia ndiye aliekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo,Robert Mwinje,mbali na kumpongeza Mbunge Mavunde pia amesema yey pamoja kamati yake ya siasa imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao.

"Pamoja na mambo mengi ambayo Mavunde ameyafanya,hili la vifaa kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi na kamati ya siasa kwa kweli tunakupongeza sana,hakika umeonyesha mfano kwa wengine,na mimi pamoja na kamati yangu ya siasa tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa uchaguzi huu tunashinda kwa kishindo."Alisema.

Vifaa vilivyokabidhiwa hii leo ni pamoja na Spika 45 zenye thamani ya shilingi 16,000,000 na Bendera 1000 zenye thamani ya shilingi 3,500,000 huku akiahidi kutoa shilingi Milioni 20,500,000 kwa mgawanyo wa Shilingi laki tano kwa kata 41 kwa lengo la kutunisha mfuko wa uchaguzi wa kata.