DC Ndejembi ampongeza Rais Magufuli kwa kuamini vijana kwenye uongozi


Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi amesema vijana nchini wanapaswa kumuunga mkono  Rais Dk John Magufuli kwa jinsi alivyowaamini kwenye nafasi mbalimbali za uongozi

DC Ndejembi amesema kwa miaka mingi ilikuepo dhana ya vijana kuonekana hawana uwezo wa kuongoza lakini Rais Magufuli katika Serikali yake ya awamu ya tano ameteua vijana wengi kwenye uongozi kuliko awamu nyingine zote.

Amesema kwa maendeleo ambayo Rais Magufuli ameyaleta ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne anapaswa kuungwa mkono na vijana na siyo kulalamika pembeni.

Ndejembi ambaye pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho kupitia Umoja wa Vijana pamoja na Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi amewataka vijana kumuunga mkono Rais Magufuli na kumsaidia kwenye utendaji wake wa kazi katika kuwatumikia wananchi.

"Mhe. Magufuli ndiye Rais wetu na ndiye Mwenyekiti wetu ndani ya Chama, mapinduzi ambayo ameyafanya kwenye Nchi hii yanapaswa kupongezwa kwa kiwango kikubwa sana.

"Leo hii chini ya Rais Magufuli Tanzania imepiga hatua kwenye sekta ya usafirishaji, tunajenga reli ya kisasa kiwango cha Kimataifa (SGR), usafiri wa anga ulikua umekufa lakini tunavyozungumza Ndege zinapishana angani kutua viwanja vya Afrika Kusini na India. Ni lazima tumuunge mkono Jemedari wetu huyu," Amesema DC Ndejembi.

Aidha ameongeza kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli Wilaya anayoiongoza ya Kongwa imeletewa zaidi ya Tsh. Bilioni 6 kwa ajili ya miradi ya maji vijijini, mtandao wa barabara ya lami unaogharimu Tsh. Bilioni 5 pamoja na mradi wa maji Kongwa ambao kiasi cha Tsh. Bilioni 1.7 kilitengwa kufanikisha mradi huo wenye lengo la kumtua Mama ndoo kichwani.