Rais Trump ataka kupunguza wanajeshi Afghanistan

Rais wa Marekani Donald Trump anataka vikosi vya jeshi la nchi hiyo nchini Afghanistan vipunguzwe hadi wakati wa uchaguzi ujao nchini humo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo alisema hayo jana, katika matamshi ambayo yanasisitiza ongezeko la shinikizo kwa Marekani kupunguza idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan.

Mkakati wa Trump katika eneo la kusini mwa Asia uliotangazwa Agosti 2017, unatoa wito wa kusitishwa upelekaji wa wanajeshi wa Marekani kwa lengo la kulishawishi kundi la Taliban kufanya mazungumzo ya amani na serikali mjini Kabul kufikisha mwisho karibu miaka 18 ya vita.

Hata hivyo, matamshi ya Pompeo yanaelekeza katika mabadiliko ambayo yamefanyika tangu mazungumzo na Taliban yalipoanza mwaka jana.